Timu ya Manchester City ya England itamenyana na vigogo wa Hispania, Real Madrid katika Nusu Fainali yao ya kwanza daima ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mabingwa wengine wa zamani wa michuano hiyo, Bayern Munich ya Ujerumani watamenyana na wakali wengine wa Hispania, Atletico Madrid.
Mechi za kwanza zinatarajiwa kuchezwa Aprili 26 na 27,wakati marudiano yatakuwa Mei 3 na 4 na City na Atletico wataanzia nyumbani. Ikumbukwe fainali ya michuano hiyo itafanyika Uwanja wa San Siro mjini Milan, Italia Mei 28, mwaka huu.
Atletico iliingia Nusu Fainali baada ya kuwato waliokuwa mabingwa watetezi, Barcelona kwa jumla ya mabao 3-2, wakishinda 2-0 Uwanja wa Vicente Calderon baada ya awali kufungwa 2-1 Uwanja wa Camp Nou, Barcelona.
Bayern Munich iliwatoa Benfica ya Ureno kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya sare ya 2-2 ugenini ikitoka kushinda 1-0 nyumbani.
Real Madrid iliwatoa Wolfsburg ya Ujerumani kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya wiki iliyopita kufungwa 2-0 Ujerumani, wakati Manchester City iliwatoa PSG kwa ushindi wa jumla wa 3-2 ikishinda 1-0 nyumbani baada ya wiki iliyopita kulazimisha sare ya 2-2 mjini Paris.