Kamati
ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limefuta
adhabu iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati
ya Saa 72) kwa viongozi na wachezaji wa Kimondo.
Kamati
ya Saa 72, ilifanya tathmini ya mchezo huo Na. 23 kati ya Kurugenzi na
Kimondo ambako iliamua kuwafungia viongozi wa Kimondo, Eric Ambakisye,
Selestine Mashenzi, na Mussa Minga kwa miezi sita na kupigwa faini ya
Sh. 500,000 kila mmoja.
Walidaiwa
kuwafuata waamuzi hotelini baada ya mechi ambapo walimpiga Mwamuzi
Mussa Gabriel na kumjeruhi wakishirikiana na baadhi ya wachezaji ambao
waliohusika katika tukio hilo wamefungiwa mechi sita na faini ya sh.
500,000 kila mmoja.
Wachezaji
waliotajwa ni January Daraja Mwamlima, Daniel Douglas Silvalwe, Abiud
Kizengo na Monte Stefano Mwanamtwa. Adhabu zote ni kwa mujibu wa Kanuni
ya 24(6) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Hata
hivyo, katika kikao chake Jumapili iliyopita, Kamati ya Nidhamu ya TFF,
chini ya Mwenyekiti Tarimba Abbas ilikubaliana na hoja ya wapinga
adhabu waliowasilisha malalamiko yao TFF mara baada ya kuadhibiwa na
Kamati ya Saa 72.
Hoja
za viongozi wa Kimondo ni kuwa hakuwahi kuitwa mbele ya Kamati hiyo
kuhusiana na jambo hilo kwa ajili ya kutoa utetezi wake na kuwa na shaka
na kamati hiyo juu ya kutoa adhabu hiyo.
Kamati
ya Nidhamu ilikubaliana na hoja hizo na hivyo kufuta adhabu hizo na
kuagiza kamati ya saa 72 ya Bodi ya Ligi Kuu kuandikia kamati ya Nidhamu
kuhusu makosa hayo ili kusikilizwa upya.