RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Anthony Mtaka kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Chama cha Riadha Tanzania (RT) - katika uongozi utakaodumu miaka minne ijayo.
Kadhalika, Rais Malinzi amewapongeza wajumbe waliochaguliwa kadhalika Baraza la Michezo la Taifa (BMT), chini ya Mwenyekiti wake, Dioniz Malinzi kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa RT, uliofanyika mjini Morogoro Jumapili.
Uongozi mpya upokee changamoto ya kuhakikisha mchezo wa riadha Tanzania unaanzia chini shuleni na unachezwa mikoa yote, tofauati na ilivyo hivi sasa inaonekana kuchezwa eneo fulani tu la Tanzania. Kadhalika wasiruhusu aina yoyote ya chembe ya migogoro.
Rais Malinzi aliwapongeza wagombea wengine waliothubutu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi lakini kwa bahati mbaya kura hazikutosha, lakini akawatia shime viongozi walioshika madaraka na kushirikiana na uongozi mpya.
Mbali ya Mtaka ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, wengine walioingia madarakani ni William Kallaghe ambaye ni Makamu wa Rais eneo la Utawala wakati Makamu wa Rais Ufundi, Dk. Ahmed Ndee huku Katibu Mkuu akiwa ni Wilhelm Gidabuday na Katibu Msaidizi ni Ombeni Zavalla.
Mweka Hazina ni Gabriel Liginyan wakati wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Lwiza John, Meta Petro, Robert Kalyahe, Dk Nassoro Matuzya, Rehema Killo, Zakaria Barie, Mwinga Mwanjala, Tullo Chambo, Christian Matembo na Yohana Misese.