Baraza la Habari nchini Tanzania
limewasilisha kesi mahakamani kupinga Sheria ya Huduma za Vyombo vya
Habari iliyopitishwa na bunge la nchi hiyo Novemba mwaka jana.
Baraza hilo linaaka baadhi ya vifungu vya sheria, ambavyo wanasema vinakandamiza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza vifutwe.
Wanasema vinakiuka matakwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo zinataka nchi wanachama kulinda haki ambazo zimeelezwa katika mkataba wa kuundwa kwa jumuiya.
"Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unahimiza umuhimu wa kufuata kanuni za utawala bora, utawala wa kidemokrasia, utawala wa sheria, uwajibikaji, uwazi, haki kwa wote, usawa wa kijinsia na kuheshimu haki za binadamu," baraza hilo linasema kupitia taarifa iliyotiwa saini na katibu mtendaji Kajudi Mukajanga.
"Tanzania inatakiwa kuchukua hatua za kuhakikisha haki zote zilizotajwa katika mkataba huo zinafuatwa na kutekelezwa."