Mashitaka ya utakakatishaji fedha inayowakabili viongozi wa zamani wa Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Mwesigwa Selestine, jana
iliahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam
mpaka Novemba 17, mwaka huu.
Mbali
na Malinzi na Mwesigwa kurudishwa rumande katika Gereza la Keko, pia
aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geoffrey Nyange
‘Kaburu’ nao walipandishwa katika mahakama hiyo na kurudishwa rumande
mpaka Novemba 17, mwaka huu.
Malinzi
na Mwesigwa, walipandishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbroad
Mashauri ambapo kutokana na upelelezi wa kesi yao kutokamilika,
wakarudishwa rumande.
Awali
upande wa utetezi wa watuhumiwa hao, uliwasilisha ombi kwa Mwendesha
Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) kuwepo mahakamani hapo ili kutoa maelezo
ya upelelezi huo ulipofikia, lakini ombi lao lilitupiliwa mbali
kutokana na kile kilichoelezwa kwamba, wakili wa serikali anavyofanya
kazi ni sawa na DPP.
Kwa
upande wa Aveva na Kaburu wanaotuhumiwa kutakatisha fedha, wakili wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai,
alisema upelelezi bado haujakamilika, hivyo kesi hiyo haiwezi
kusikilizwa kwa sasa.
Hakimu
Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Victoria Nongwa ambaye ndiye
anasikiliza kesi hiyo, aliutaka upande wa mashitaka kufanya haraka
katika upelelezi wao ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.