Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sasa linaonekana halitakuwa na utani linapofikia suala la bima kwa wachezaji.
Mara kadhaa, suala hilo la bima limekwua likisisitizwa lakini bila ya mafanikio na klabu huona ni kama mzaha fulani hivi.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Wallace Karia leo amesema kamwe hataruhusu klabu yoyote kucheza
Ligi Kuu Bara kama itakuwa haijawakatia bima wachezaji wake.
Karia amesema hilo litaanza kwa msimu ujao wa 2018/2019 na hakutakuwa na msamaha.
Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa
semina ya utawala bora kwa klabu za ligi kuu na Ligi Daraja la Kwanza
iliyofanyika jana Rombo Green View iliyokuwepo Ubungo jijini Dar es
Salaam ambayo ilihusisha klabu kongwe za Simba na Yanga.
Semina hiyo, iliandaliwa na Kampuni ya
Maendeleo na Utafiti wa Michezo (ISDI) kwa kushirikiana na Alliance Life
Assuarance na TFF kwa lengo la kutoa elimu kwa viongozi wa klabu kujua
jinsi ya utawala, kujiongoza na kutafuta wadhamini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kabla
ya kufungua semina hiyo, Karia alisema kikubwa anataka kuona klabu
maendeleo na mafanikio kwa klabu hizo huku akiamini kupitia semina hiyo
wawakirishi hao watapata elimu nzuri.
“Hakutakuwa na utani juu la hili la bima
ni lazima kila klabu iwakatie bima ya afya wachezaji wake na uzuri wapo
hapa Alliance Life Assuarance ambao wanausika na bima.
“Kama klabu haitakuwa imewakatia bima
wachezaji wake, basi haitacheza ligi kuu msimu ujao na hilo
nitahakikisha ninalisimamia vizuri na kama itakuwepo klabu imeshindwa
kutimiza hilo basi itatakiwa kuwasiliana na bodi ya ligi tujue jinsi ya
kuwasaidia ili wakatiwe bima,” alisema Karia.