Mwenyekiti wa chama cha upinzani
nchini Tanzania Chadema amesema kama chama hawana imani na watendaji wa
mahakama licha ya kwamba wanaiheshimu kama "muhimili muhimu wa taifa ."
Mwanasiasa huyo pia amevituhumu vyombo vya dola akisema vimekuwa vikishiriki katika kupanga na kutekeleza mashambulizi mbalimbali ya kudhoofisha demokrasia nchini Tanzania.
Akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho, Bw Mbowe alitolea mfano tukio la hivi karibuni la jeshi la Polisi kutumia risasi za moto kuwakabili waandamanaji wanachama wa chama hicho ambao "hawakuwa na silaha za aina yoyote."
Mbowe aliyekuwa amaembatana na viongozi wengine wa juu wa chama hicho amesema wanaungana na Chama cha Wananchi CUF kuituhumu tume ya taifa ya Uchaguzi NEC pamoja na ZEC katika kupindisha uchaguzi na kuchochea uchaguzi usio wa haki.
Baada ya mkutano huo, Bw Mbowe na wenzake sita waliitika wito wa jeshi la polisi na kwenda kuripoti polisi.
Walikuwa wakikubali wito waliopewa siku za hivi karibuni baada ya uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kinondoni uliopelekea maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo kikuu Akwilina Akwiline.
Watanzania wanasemaje kuhusu kufungwa kwa Joseph Mbilinyi?
Hatua ya kufungwa jela kwa Bw Mbilinyi na Katibu wa Chadema Kanda ya nyanda za juu kusini, Emmanuel Masonga imepokelewa na baadhi ya Watanzania mtandaoni kwa mshangao.
Baadhi, kama vile Evarist Chahali wametazama hiyo kama ishara ya dalili za utawala wa kiimla.