kikao cha Leo kati ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Uongozi wa Yanga chini ya Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, maafikiano yamefikiwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Yanga uendeshwe na Yanga wenyewe.
Taarifa ya TFF iliyosambazwa na TFF kupitia Ofisa Habari wake, Alfred Lucas, ilisema: “Maamuzi yaliyotoka ni kwamba, uchaguzi wa Yanga umebarikiwa kuendelea kama ulivyopangwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kwamba utafanyika June 11, 2016 chini ya uangalizi wa kamati ya uchaguzi ya TFF.”
TFF imesema Wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo ambao walichukua fomu TFF, kikao hicho cha Leo kimeamua kiwarudishe Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kuendelea na taratibu zilizopo za uchaguzi endapo wanakidhi vigezo vya uchaguzi vya Kamati ya Uchaguzi ya Yanga.
Kabla ya maelewano haya kulikuwa na mvutano mkubwa ambapo Yanga walitangaza mchakato wa Uchaguzi wao wenyewe ambao walipanga ufanyike Juni 11 huku TFF ikitangaza uchaguzi huo huo ni Juni 25 na kila upande ulitoa Fomu kwa Wagombea.